Ni wiki ya Mbarawa, Mwakyembe bungeni
MKUTANO wa Bunge la 11 unaendelea leo, ambapo Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2018/19, yanatarajiwa kuwasilishwa. Wizara hiyo inaongozwa na Profesa Makame Mbarawa.
Baada ya bajeti hiyo ya Wizara ya Ujenzi, Aprili 27 siku ya Ijumaa itakuwa zamu ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, inayoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe.
Katika mkutano huo wa leo bungeni, hoja za miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara mbalimbali nchini, ununuzi wa ndege za serikali na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), zinatarajiwa kuibua mjadala mkali bungeni humo.
Kwa sasa wizara hiyo inatekeleza miradi mbalimbali ya miundombonu ikiwemo ujenzi huo wa SGR, barabara za juu kwa ajili ya kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam na ujenzi wa barabara mbalimbali za kuiunganisha Tanzania na nchi za jirani.
Aidha, wizara hiyo inagusa maeneo nyeti ya biashara ikiwemo bandari mbalimbali, zinazotoa huduma nchini na kwa nchi za jirani, ambazo hazijapakana na bahari.
Pamoja na hayo, majadiliano hayo bungeni pia yanatarajiwa kugusa maendeleo ya matumizi ya simu za mkononi, mitandao ya kijamii ikiwemo kanuni mpya za matumizi ya mitandao, ambazo zinawataka wamiliki wake kujisajili na kulipia mitandao.
Kuhusu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambayo siku ya Ijumaa itawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19, majadiliano yanatarajiwa kugusa maeneo ya uhuru wa habari, haki za wasanii ikiwemo suala la kufungiwa kwa baadhi ya nyimbo za wasanii kutokana na kwenda kinyume na maadili na utamaduni wa Mtanzania.
Bunge litapumzika kwa siku moja Alhamisi Aprili 26, mwaka huu, kupisha maadhimisho ya Siku ya Muungano, ambayo yatafanyika kitaifa mjini Dodoma na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Magufuli.
Wiki iliyopita Bunge hilo lilipitisha Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Comments
Post a Comment