Tanzania kushiriki tamasha la Utalii

TANZANIA inatarajiwa kushiriki katika Tamasha la Urithi wa Utamaduni wa Mabara linalotarajiwa kufanyika kwa siku nne katika mji wa Cherbourg, Ufaransa. Tamasha hilo ambalo ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushiriki, linatarajiwa kufanyika Julai mwaka huu na litatoa fursa kwa Tanzania kutangaza vivutio vyake.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha wadau mbalimbali wanaohusika na tamasha hilo.
Amesema, watalii kutoka nchi mbalimbali watakuja nchini na kwamba litahusisha nchi zote za Afrika na kwamba limelenga kutangaza tamaduni na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika mataifa yote yatakayoshiriki huku likitajwa kuwa tamasha bora na kubwa la utalii pengine kuliko matamasha mengine yote kutokana na kila nchi kujitokeza na kuonesha vivutio vinavyopatikana katika mataifa yao.
“Tanzania tunavyo vivutio mbalimbali tunavyotarajia kwenda kuvionesha katika tamasha hilo, ukiacha vivutio vya mambo ya kale, tuna bonde la Olduvai Gorge na mengineyo tunayoamini kuwa kupitia tamasha hilo tutaweza kuyatangaza na hivyo kuvutia watalii wengi kuja nchini,” amesema Dk Kigwangalla.
Aidha alisema tamasha hilo la mabara ni kama salamu ya ujio wa tamasha la ‘Urithi wetu’ linalotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini Septemba mwaka huu, maalumu kwa ajili ya kuiwezesha mikoa yote kutangaza mambo mbalimbali ya utalii yanayopatikana katika mikoa hiyo.
Alisema tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika kwa kipindi cha mwezi mzima, pia litatoa fursa kwa kila wilaya kutangaza vivutio vyake, huku akizitaka kila wilaya kujiandaa na tamasha hilo, litakalotoa fursa pia kwa mikoa na wilaya hizo kujikuza kiutalii.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Profesa Audax Mabula, alisema tamasha la urithi mbali na mambo mengine, litazisaidia wilaya zitakazoshiriki kujitangaza kwa hatua mbalimbali huku akisisitiza kuwa hiyo ni fursa pekee itakayozidi kutangaza utalii kuanzia ngazi za chini.
Aidha alisema Tanzania inazidi kupiga hatua katika eneo la utalii kutokana na jitihada mbalimbali inazozifanya kutangaza vivutio vyake na hivyo kuwavutia watalii kutoka mataifa mbalimbali kufika kwa lengo la kujionea vivutio hivyo.

Comments

Popular Posts