VIDEO-JPM achambua changamoto Jumuiya Afrika Mashariki

Rais John Magufuli amesema wabunge wa Afrika Mashariki wamechaguliwa katika kipindi ambacho jumuiya hiyo imepiga hatua kubwa kimaendeleo lakini inakabiliwa na changamoto nyingi.
Akihutubia Bunge la Afrika Mashariki (Eala) jana mjini hapa, Rais Magufuli alisema ukanda wa Afrika Mashariki unasifika kwa ukuaji wa uchumi, huku nchi hizo zikiondoa vikwazo vya uchumi na uwekezaji.
Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto katika jumuiya hiyo, “Bado inakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo nyinyi wanajumuiya ya Afrika Mashariki mna jukumu la kuzishughulikia. Tuna tatizo la migogoro ambayo nyinyi mnaifahamu.”
Alisema migogoro hiyo imekuwa ikigharimu maisha ya watu wengi.
Alisema changamoto nyingine ni vikwazo vya kibiashara na uwekezaji, “Lakini pia kutoaminiana ndani ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mara nyingi hatupendi kuyasema sema haya lakini mimi ninayasema ili muijue hiyo ‘challenge’ (changamoto).”
Aliwataka waanze kuziondoa changamoto hizo kwani umoja wao unatakiwa kuwa kama walivyo marais wa Jumuiya hiyo.
“Mawaziri, wabunge, watendaji wote na baadaye wananchi wote na nyinyi kama wabunge wa jumuiya ya Afrika Mashariki, mna jukumu la kuzimaliza, tupendane, tujione ndugu,” alisema.
Kadhalika Rais Magufuli aliwataka wabunge wa hao kuhakikisha wanajenga umoja kwa kuaminiana na kupendana miongoni mwa wanachama.
Alisema wanachama wa jumuiya hiyo wana imani na wabunge hao na kuwaomba wasiwaangushe.
Alisema jukumu ni kuleta maendeleo ya wananchi wanaowaongoza na kwamba wakianza wao kuwa na changamoto, watashindwa kuwasaidia wananchi ambao wanawaongoza.
Aliwataka viongozi wa Jumuiya hiyo kushughulikia miradi inayokuja kwa kasi; “Mmekuwa na spidi ndogo katika kushughulikia miradi mbalimbali ukiwamo wa Malindi Horohoro hadi Bagamoyo, sasa ni zaidi ya miaka kadhaa licha ya kufanyika upembuzi yakinifu sijamuona mkandarasi nimechomekea ili na yeye aondoke na meseji.”
Rais pia aliwahakikishia aliwahakikishia wabunge hao kuwa Tanzania inaendelea kushirikiana na nchi zote na wanachama wote wa jumuiya hiyo katika kutimiza dira na malengo yake.
“Yale maamuzi mengine yanayochelewachelewa nataka kuwahakikishia tutayapeleka spidi kwelikweli ili yawe na masilahi mapana katika Afrika Mashariki.
“Tusipelekeshwe na wengine, ni lazima katika maamuzi yote tuwe tunafanya evaluation (tathmini) ya kutosha hasa katika mikataba tunayoingia na wasiokuwa wanachama wa jumuiya yetu,” alisema.
Aliwataka wabunge wa jumuiya hiyo kuwapa elimu wananchi na kuwatahadharisha juu ya watu wenye nia mbaya na umoja huo.
Mkutano huo wa wiki tatu unaongozwa na Spika wa Bunge hilo, Martin Ngoga na utajadili miswada na maazimio mbalimbali.
Miswada itakayojadiliwa ni pamoja na Itifaki ya Sarafu Moja ambao ni mswada wa taasisi ya Fedha na mswada wa Takwimu, yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2017.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mbunge wa jumuiya hiyo kutoka Uganda, Denis Namala alisema watahakikisha programu ambazo Rais Magufuli amezizungumza zinatekelezwa kwa manufaa ya wana jumuiya wa Eala.

Comments

Popular Posts