Vituo tiba dawa za kulevya kuchunguzwa
SERIKALI imetangaza vita dhidi ya wamiliki wa vituo vya kutibu waathirika wa dawa za kulevya wanaofanya mchezo wa kuwachoma kwa makusudi sindano wagonjwa waliopata nafuu ili waendelee na tiba kwenye vituo hivyo, kuwa kuanzia sasa watachunguzwa na wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Hayo yalibainishwa bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu, Halima Bulembo (CCM).
Katika swali lake mbunge huyo alisema kuna malalamiko kuwa baadhi ya vituo hivyo vinavyotoa tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya, vinavyowachoma kwa makusudi sindano wagonjwa waliopata nafuu ili waendelee na tiba vituoni humo kwa ajili ya kupata fedha zaidi.
Akijibu swali hilo, Waziri Mhagama alikiri kuwa serikali imepokea taarifa za kuwepo kwa baadhi ya vituo vinavyofanya mchezo huo mbaya kwa ajili ya kujinufaisha jambo ambalo linazidi kukandamiza juhudi za serikali katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini.
"Naagiza wamiliki wote wa vituo hivi wanaoendeleza tabia hii waache haraka lakini pia naziagiza mamlaka zinazohusiana na masuala ya afya kufanya uchunguzi wa kina na kituo kitakachobainika kichukuliwe hatua za kisheria," alisisitiza.
Awali, akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Anthony Mavunde, alikiri kuwa kwa sasa asilimia kubwa ya vituo hivyo vinavyotoa tiba ya waathirika wa dawa za kulevya vinamilikiwa na watu binafsi.
Katika swali la msingi la mbunge Chumbuni, Ussi Salum (CCM) Pondeza alitaka kujua lini serikali itachukua hatua dhidi ya wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya wanaoingiza na kuuza dawa hizo badala ya kuwakamata waathirika wanaohitaji misaada na ushauri wa kuachana na matumizi ya dawa hizo.
Akijibu swali hilo, Mavunde alisema serikali imejipanga kukabiliana na wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa dawa za kulevya ambao wote wanasababisha madhara kwa jamii kwa kufanya biashara hiyo.
"Hadi kufikia Februari, mwaka huu jumla ya wafanyabiashara 3,486 wa dawa hizo walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Kati ya hao zaidi ya asilimia 30 ni wafanyabiashara wakubwa," alieleza.
Mwenyekiti wa Bunge hilo na Mbunge wa Ilala, Musa Zungu (CCM) alitaka suala hilo la dawa za kulevya lipigwe vita na wananchi wote kutokana na ukubwa wake na isiachiwe serikali pekee.
Comments
Post a Comment