DC Hapi ‘awachana laivu’ trafiki Kinondoni

Mkuu wa wilaya ya Kinondoni,Ally Hapi

Mkuu wa wilaya ya Kinondoni,Ally Hapi akiangalia karavati la kupitishia maji ya mvua kuelekea baharini, lililopo eneo la Masana, Dar es salaam. 
Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema askari wa usalama barabarani wanaosimama eneo la  Daraja la Bondeni, Tegeta hujitengenezea ‘ulaji’ kwa kisingizio cha madereva kuendesha spidi ya kilometa 30 jambo ambalo ni kinyume na kisheria.
Hapi amesema hayo leo Mei 31, alipokuwa kwenye ziara ya kutembelea miradi ya barabara pamoja na madaraja inayogharimu zaidi ya Sh20 bilioni.
 Miradi hiyo inasimamiwa na  Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
Hapi amewataka askari hao waache mara moja  la sivyo atawachukulia sheria.
"Tanroads  wameweka vibao vya kuendesha spidi 30 kwa lengo la kuwajulisha madereva wapunguze mwendo kwa kuwa kuna ujenzi unaendelea lakini hawa askari wa usalama barabarani wamekuwa wakijificha kwenye kona na darajani hapo na kuwakamata madereva  na wakiwatoza fedha nyingi jambo ambalo siwezi kukubaliana nalo,"amesema Hapi.
Amesema askari polisi hao hujificha ili kuwavizia madereva wa magari na kuwaeleza kuwa wameendesha kwa zaidi ya spidi 35 wakati kisheria haijawa rasmi  kudhibiti mwendo huo kama wanavyodai.
Pia ameiomba Tanroads na wizara husika kuweka barabara ya mwendo kasi kwa awamu ya tatu badala ya nne kama walivyopanga kwa kuwa barabara ya Bagamoyo ina msongamano mkubwa wa magari .
Akizungumzia miradi hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mipango Tanroads, Mkoa wa Dar es Salaam, Elisony Mweladzi amesema wanaendelea na ujenzi wa Daraja la Mlalakuwa litakalogharimu Sh4.8 bilioni na ujenzi wa daraja waenda kwa miguu eneo la bondeni utagharimu Sh1.9 bilioni.

Comments

Popular Posts