Mbunge CCM ataka mawaziri wa madini waende kwa ‘sangoma’

Mbunge wa Newala Vijijini, Ajali Rashid Akibar

Mbunge wa Newala Vijijini, Ajali Rashid Akibar akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. 
Dodoma. Mbunge wa Newala Vijijini (CCM), Ajali Akibar amewataka mawaziri wa madini kwenda Afrika ya Kusini kuwatafuta ‘masangoma’ (waganga wa kienyeji) wathibitishe kama kweli madini yanatokana na majini ili Watanzania waipate kwa wingi rasilimali hiyo.
Akichangia  bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2018/19, leo Mei 31, Akibar amesema kuwa hadhani kama Rais John Magufuli ameipenda  wizara hiyo kwa kuipa mawaziri watatu bali anataka ilete matokeo mazuri.
“Nimewahi kusikia kuwa madini yanatokana na majini kama ni kweli muende South Afrika (Afrika Kusini) mkatafute sangoma ili na sisi tupate madini,”amesema.
Amesema kutokana na utendaji mbovu wa Shirika la Madini Nchini (Stamico) angekuwa yeye angelivunja shirika hilo kwa kushindwa kufanya kazi.
“Stamico itaendelea kuwa mzigo kwetu, tuivunje,” amesema.
Kauli ya kutaka Stamico ivunjwe iliungwa mkono na Mbunge wa Manonga (CCM) Seif Gulamali ambaye amesema kuwa waendelee kuipa fedha kwa majaribio.
Amesema badala ya shirika hilo kuleta  faida  linaleta hasara huku kampuni binafsi za madini zikizalisha faida.

Comments

Popular Posts