Yusuf Makamba: Mlima umekwenda makao makuu ya CCM



Dar es Salaam. Katibu mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba anajulikana kwa hadithi, misemo na methali nyingi anapotaka kueleza jambo lake kirahisi.
Na amefanya hivyo kuzungumzia uteuzi wa katibu mkuu mpya wa CCM, Dk Bashiru Ally Kakurwa alipoulizwa maoni yake kuhusu mabadiliko hayo. “Historia inajirudia,” alisema Makamba jana.
Alisema awali Pius Msekwa, ambaye alikuwa Spika wa Bunge alikuwa katibu mtendaji mkuu wa Tanu, baadaye akateuliwa kuwa makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Mwandishi wa habari wa gazeti la Serikali wa wakati huo, Philip Ochieng aliandika ‘Tanu goes to the hill’ (Tanu imekwenda mlimani). Sasa hivi imekuwa ‘the hill goes to the CCM headquarter’ (Mlima unakwenda makao makuu ya CCM,” alisema bila ya kufafanua, lakini akiangua kicheko. “Ningekuwa mwandishi ningeandika hivyo mimi. Mzee Msekwa akiiona hii imeandikwa atafurahi sana, kwa sababu atakuwa ameisahau kwa kuwa ni muda mrefu.”
Fumbo lake laweza kutafsiriwa kwa maana tofauti, lakini anaweza kuwa alimaanisha kuwa enzi hizo Msekwa alipoteuliwa kuwa mtendaji mkuu wa Tanu, chama hicho kilikuwa kama kimemfuata mtu aliyeshika nafasi ya juu kuwa mtendaji mkuu na sasa mtu msomi amekwenda CCM.
Kuhusu Dk Bashiru, Makamba alisema ni kiongozi kijana anayeijua CCM na kwamba kazi ya kuhakiki mali za chama hicho imempa fursa ya kukijua zaidi.
“Ameziona mali za chama na fursa zilizopo ndani ya CCM. Atakisaidia sana chama hiki. Narudia tena kumpongeza Dk Magufuli na wajumbe wa NEC,” alisema Makamba.
Pia alimpongeza, katibu mkuu aliyestaafu, Abdulrahman Kinana akisema alisoma alama za nyakati.
Alisema Kinana ameondoka wakati muafaka kwa sababu wanachama bado wanampenda, badala ya kusubiri wamchoke.
“Usingojee waanze kuguna. Mimi nilichelewa kutoka ndio maana watu wakaanza kusema mbona huyu mzee hatoki wakati vijana wapo?” alisema Makamba.

Comments

Popular Posts