Kamati yaitaka TRA kufanya utafiti bei ya nguo zinazoagizwa nje ya nchi
Dodoma. Kamati ya Bunge ya Bajeti imeishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya utafiti ili kupata bei halisi ya nguo zinazoagizwa kutoka nje ili kutoza kodi stahiki na kulinda viwanda vya ndani.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Ghasia akiwasilisha maoni ya kamati bungeni leo Juni 28, 2018 amesema kamati ilipata fursa ya kukutana na wamiliki wa viwanda vya nguo nchini ambao wanatumia pamba kutengeneza nguo.
Amesema changamoto waliyoibainisha wamiliki hao ni kuwa nguo zinazoingizwa nchini (takribani asilimia 85 ya nguo zote) zinatozwa kodi ndogo na hivyo kuuzwa kwa bei ya chini ikilinganishwa na nguo zinazotengenezwa na viwanda vyetu hapa nchini.
Ghasia ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Vijijini(CCM)amesema sababu ya nguo za ndani kuuzwa bei ya juu ni kutokana na gharama za uzalishaji (uchakataji) kuwa juu hivyo kusababisha nguo zetu kuonekana ghali na hivyo kushindwa kuuzika.
“Kamati inaishauri Serikali kupitia TRA ifanye utafiti na kupata bei halisi ya nguo zinazoagizwa kutoka nje na hivyo kuwa na msingi kwa ajili ya kutoza kodi stahiki hivyo kulinda viwanda vyetu vya ndani vinavyozalisha nguo kupitia malighafi ya pamba,” amesema Ghasia
Comments
Post a Comment